Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam la Kanisa Katoliki,Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo
KWA mara nyingine, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam la Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ameonyesha kukerwa na kauli ya kufumbafumba aliyoitoa Rais Kikwete akiwahusisha viongozi wa dini na biashara ya dawa za kulevya.
Baada ya kufanya hivyo katika kipindi kisichozidi wiki mbili, Kardinali Pengo alirejea tena wito wake jana, akimtaka Rais Kikwete kuwataja hadharani viongozi wa dini ambao aliwatuhumu kujihusisha na biashara hiyo.
Tofauti na ilivyokuwa wakati alipozungumza kwa mara ya kwanza, katika kauli yake ya jana, Pengo alikifananisha kitendo cha Rais Kikwete kushindwa kuwataja kwa majina viongozi wa kiimani anaowashutumu na usaliti.
“Kiongozi mwenye uchungu na mzalendo kwa taifa hana budi kutaja majina ya watu wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali kwa masilahi ya taifa na wananchi kwa ujumla… yeye kushindwa kufanya hivyo ni msaliti wa nchi,” alisema.
Kiongozi wa nchi wa kweli haoni haya kutaja mafisadi, au wala rushwa hadharani. Endapo anaona haya kuwataja ni msaliti ndani ya nchi yake,” alisema Pengo.
Pengo alikwenda mbali zaidi na akamfananisha kiongozi mwenye uzalendo na nchi kuwa sawa na mwanamke mjamzito anayeshikwa na uchungu wa kuzaa wakati akiwa mbele ya nyoka mwekundu.
Alisema kuwa mwanamke wa namna hiyo huendelea na uzazi pasipo kujali au kuhofia hatari ya nyoka aliyeko mbele yake.
Pengo alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza katika ibada maalumu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Kristo Mfalme, Tabata jijini Dar es Salaam jana.
Kardinali Pengo, mmoja wa viongozi wa dini wanaoheshimika, alisema kitendo cha Kikwete kutoa tuhuma hizo nzito wakati akiwa katika shughuli ya Wakatoliki kinaweza kutafsiriwa kuwa alikuwa akiwalenga wao ambao walikuwapo katika hafla hiyo.
Rais Kikwete alitoa tuhuma hizo ambazo zimeibua manung’uniko ya wazi kutoka kwa viongozi wa Kikristo wakati wa ibada maalumu ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu wa Jimbo la Mbinga, Mhashamu John Ndimbo.
“Rais Kikwete hakupaswa kutumia jukwaa la Wakatoliki kutoa kauli hiyo. Angeweza kutumia sehemu nyingine ili tuliokuwepo tusijione kuwa walengwa wa ujumbe,” alisema Kardinali Pengo.
Pengo anakuwa ni kiongozi wa pili wa juu wa Kikristo kutoa kauli hiyo kali, baada ya Umoja wa Maaskofu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania, (CCT) kumpa Rais Kikwete saa 48 za kuwataja kwa majina viongozi wanaotuhumiwa kwa biashara ya dawa za kulevya.
Tamko hilo la maaskofu wa CCT ambalo hata hivyo halikujibiwa na Kikwete hadharani zaidi ya majibu yasiyo na majina kutolewa na viongozi wengine, lilisomwa mbele ya wanahabari mwanzoni mwa mwezi Julai na Mwenyekiti wao, Askofu Peter Kitula.
“Tunampa saa 48 rais awataje kwa majina viongozi hao ambao yeye anadai wanajihusisha kuuza dawa za kulevya na kama atashindwa kufanya hivyo tutatafsiri kuwa ni kiongozi mwongo na mzushi.
“Tunasikitishwa na kushangazwa kwa kauli hiyo na tunamheshimu kama kiongozi wa nchi, hivyo tunampa muda huo (saa 48) awataje kwa majina,” alisema Askofu Kitula.
Akiwa Mbinga wakati wa sherehe hizo za kuwekwa wakfu kwa askofu mpya, Rais Kikwete alieleza kusitikitishwa na hatua ya viongozi wa kidini kujihusisha na biashara hiyo ya dawa za kulevya.
“Inasikitisha sana na kutisha biashara hii haramu sasa inawavutia hata watumishi wa Mungu. Taifa letu litaharibika tusipokuwa makini katika hili, baadhi yenu tumewakamata.
“Kwa kauli zenu kemeeni jambo hili kwa kuelimisha jamii hususan vijana waweze kuepukana na matumizi ya dawa za kulevya,” alisema Kikwete pasipo kufafanua.
No comments:
Post a Comment