katibu Mkuu kiongozi, Mr Luhanjo
IKULU imemrejesha kazini Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo baada ya uchunguzi wa tuhuma dhidi yake za kutenga mamilioni ya shilingi kwa ajili ya kuhonga wabunge ili wapitishe bajeti ya wizara hiyo, kubainika kuwa si za kweli.Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo alitangaza uamuzi huo katika mkutano wake na waandishi uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam jana akisema Jairo hana hatia na leo anapaswa kurejea kazini mara moja.
Alisema matokeo ya uchunguzi dhidi yake yamebainisha kwamba hakuwa na hatia hivyo kusema kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa Sheria namba 8 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2003, anamrejesha kazini Jairo... “Ninaamuru David Jairo arejee kazini kuanzia siku ya Jumatano (leo).”
Julai 18, Jairo alituhumiwa na baadhi ya wabunge wakati wakichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwamba amezitaka taasisi, vitengo na idara zilizo chini ya wizara hiyo, zichangie Sh50 milioni kila moja, ili kufanikisha bajeti hiyo.
Tuhuma hizo zilitolewa na Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo na kumfanya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuzitolea maelezo Bungeni akisema akama angekuwa na mamlaka, angelitolea uamuzi lakini akaahidi kulifikisha kwa Rais ambaye alisema ndiye mwenye mamlaka ya uteuzi.
Tuhuma nyingine zilizokuwa zimetolewa na Shellukindo ni za kulipa masurufu ya safari za watumishi walio chini ya wizara hiyo na taasisi zake, ambao tayari walikwishalipwa na wizara na taasisi hizo.
Kutokana na tuhuma hizo Luhanjo alimpa likizo ya malipo katibu huyo na Julai 21 alimwandikia barua Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovic Utouh na kumpa siku 10 kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo ambao alisema haukuweza kuthibitisha tuhuma hizo.
Luhanjo ambaye katika mkutano huo wa waandishi alikuwa na Utouh alisema: “Kutokana na matokeo haya ya uchunguzi wa awali, mimi kama Mamlaka ya Nidhamu ya Katibu Mkuu Nishati na Madini (Jairo), sitaweza kuendelea na hatua ya pili ya kumpa taarifa ya tuhuma. Pia sitampa Hati ya Mashtaka kwa sababu Jairo hajapatikana na kosa la kinidhamu kwa mujibu wa taarifa za ukaguzi maalumu.”
Luhanjo alisema mantiki na shabaha ya uchunguzi wa awali dhidi ya mtumishi wa umma anayetuhumiwa ni matakwa ya kisheria kwa mujibu wa Kanuni ya 36 ya Kanuni za Utumishi wa Umma ya mwaka 2003.
“Lengo la kwanza ni kupata ukweli kuhusu tuhuma zinazohusika, pili ni kutaka kubaini kama mtumishi ametenda kosa la kinidhamu.
Tatu, kama uchunguzi huo utabainisha makosa ya kinidhamu, mamlaka ya nidhamu itampa mtumishi taarifa muhimu ambayo itaambatana na Hati ya Mashitaka,” alisema.
Akizungumzia madai ya rushwa, Luhanjo alisema tuhuma hizo zisingeweza kuchunguzwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), kwa kuwa hazihusiani na masuala ya utoaji na upokeaji rushwa.
“Kila chombo kina nafasi yake… kama mtu akiona katika ripoti kuna mianya ya rushwa suala hili linaweza kufika Takukuru, Polisi na hata Mahakamani,” alisema Luhanjo.
Alisema ni kawaida kwa idara zilizo chini ya wizara husika kuchanga fedha kwa ajili ya kusaidia kufanikisha kitu fulani, huku akisita kuzungumzia kuchafuliwa kwa jina la Jairo akidai suala hilo ni la binafsi na ndiye anayepaswa kulizungumzia.
“Jairo kuomba taasisi zilizo chini ya wizara ya nishati kumwezesha kufanikisha bajeti ya wizara ni jambo la kawaida, kwa kuwa bajeti hiyo pia huzihusisha taasisi zilizopo chini ya wizara husika,” alisema Luhanjo.
Aonya watumishi wa umma
Luhanjo aliwaonya watumishi wa Serikali wanaotoa siri huku akisema kufanya hivyo ni kuvunja kiapo cha kutunza siri za Serikali.
“Nawaonya watumishi wa umma wanaotoa siri za Serikali…, tutafuatilia tujue nani alitoa barua kwa mbunge, akipatikana atapewa adhabu,” alisema Luhanjo.
Uchunguzi wa CAG
Awali, akisoma matokeo ya uchunguzi huo, Utouh alisema:
“Kazi hii ya uchunguzi ilihusisha vitabu na risiti, hati za malipo na taarifa za benki kwa kipindi cha Mei hadi Julai 2011. Timu ya ukaguzi iliwahoji watu mbalimbali kutoka taasisi zilizochangishwa, wizara, wabunge na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST).”
Alisema ukaguzi ulibaini kuwa idadi ya taasisi zilizopelekewa barua za kuchangia gharama za kuwasilisha bungeni bajeti ya wizara hiyo ni nne na siyo 20 kama tuhuma zilivyodai.
Utouh alizitaja taasisi hizo kuwa ni Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Tanesco, TPDC, Ewura, Idara ya Uhasibu na Idara ya Mipango ya Wizara ya Nishati na Madini. Alisema pia ukaguzi umebaini kuwa jumla ya fedha zilizochangwa kutoka kwenye taasisi zilizochangishwa ni Sh149,797,600.
“Wakati huohuo Idara ya Uhasibu ya Wizara ilichangia Sh150,720,000 kwa ajili ya posho za vikao vya kazi katika uandaaji wa uwasilishaji wa bajeti ya wizara,” alisema Utouh.
CAG Utouh alisema Idara ya Mipango ya wizara ilichangia Sh278,081,500 kwa ajili ya gharama ya uwasilishaji wa bajeti ya wizara, huku Tanesco ikichangia Sh40,000,000 na TPDC Sh50,000,000... “Jumla ya michango yote ni Sh 578,599,100 na siyo bilioni moja iliyotajwa kwenye tuhuma.”
Alisema taasisi moja (Ewura) haikutuma mchango wake kama ilivyokuwa imeagizwa, bali ilijitolea kugharamia chakula cha mchana cha kiasi cha Sh3,656,000 kilicholipwa kwa kampuni ya African Conference Centre, Julai 18, mwaka huu.
“Pia taasisi hii ililipia gharama za tafrija iliyofanyika Julai 18 jioni katika Ukumbi wa St Gasper Dodoma kwa gharama ya Sh6,141,600, pamoja na kuwa bajeti haikupita, tafrija ilifanyika kwa kuwa maandalizi yalishafanyika na hata gharama ingelipiwa tu,” alisema Utouh.
Wabunge kuhongwa
Alisema ukaguzi maalumu haukupata ushahidi wowote wa fedha zilizochangwa kutumika kuwalipa wabunge ili bajeti hiyo ipitishwe kirahisi.
“Timu ya ukaguzi ilitumia mbinu mbalimbali zikiwamo zile za mifumo ya kieletroniki ya kuchambua data (CAATS) na kupata jumla ya malipo kwa kila ofisa aliyelipwa katika mchakato wa kuwasilisha bajeti,” alisema Utouh.
CAG alisema katika uchambuzi huo, imebainika kwa uhakika kuwa malipo yaliyofanyika yalihusu posho ya kujikimu, takrima na posho za vikao kwa maofisa walioshiriki katika shughuli nzima ya kuwasilisha bajeti ya wizara na kwamba hakuna ushahidi wa malipo kwa wabunge.
Taarifa ya benki
Alisema taarifa ya benki ya Julai 29, mwaka huu kuhusu akaunti namba 505100068 ya GST iliyotumika kukusanya fedha zilizochangwa inaonyesha kuwa jumla ya Sh99,438,380 zilirejeshwa kwenye akaunti hiyo Julai 20.
“Pia taarifa hiyo ya benki inaonyesha kuwa kiasi cha Sh14,860,000 kilirejeshwa kwenye akaunti hiyo Julai 27. Hii ni baada ya kupitia vitabu vya hesabu vya GST pamoja na kuwahoji wahusika,” alisema Utouh,
“Ilibainika kuwa kiasi cha Sh99,438,380 kilisalia kutokana na fedha za kuwasilisha bajeti ya wizara bungeni na zilipokewa Julai 27, pia ilibainika kuwa kiasi cha Sh14,860,000 kilikuwa ni bakaa (akiba) ya fedha za kikao cha kazi cha kuandaa uwasilishaji wa bajeti, fedha ambazo zilipokewa Julai 27.”
Utouh alisema mpaka siku ya ukaguzi Julai 29, akiba ya fedha zilizochangwa kwa ajili ya kuiwasilisha bajeti bungeni ilikuwa Sh195,235,567.33.
Alisema kati ya hizo, Sh20,000,000 ni akiba ya matumizi ya fedha zilizochangwa na kupokewa kwenye akaunti ya GST kabla ya kufanyika marejesho ya Sh99,438,380 na Sh14,860,000.
Alisema Sh99,438,380 zilirejeshwa benki baada ya mchakato wa bajeti kukwama na kusogezwa mbele ambazo zinatokana na mchango wa Idara ya Mipango ya Wizara na taasisi nyingine zilizofikia Sh418,081,500.
Alisema Sh14,860,000 zilirejeshwa katika akaunti zikiwa ni akiba ya fedha za kikao cha kazi cha matayarisho ya uwasilishaji wa bajeti ya wizara ambazo zilikuwa hazijatumika kutokana na kwamba zilikuwa ni mchango wa Idara ya Uhasibu ya wizara wa Sh 150,720,000 kwa ajili ya vikao vya kazi mjini Dodoma.
“Kiasi cha Sh60,937,167 ambazo na masalia ya fedha za GST zikiwa ni fedha za matumizi ya kawaida ya taasisi, kulingana na taarifa za kibenki ya Julai 29, fedha ni Sh195,235,537, zikijumlisha kiasi cha Sh60,937,167 ambazo ni fedha za GST za matumizi ya kawaida ” alisema Utouh.
No comments:
Post a Comment