SERIKALI imekubali pendekezo la kutafakari na kuziangalia upya posho mbalimbali wanazolipwa watumishi wa umma, wakiwamo wabunge.
Uamuzi huo wa Serikali ulitangazwa bungeni jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati alipokuwa akihitimisha mjadala wa makadirio na matumizi ya ofisi yake uliodumu kwa wiki moja.
Pinda alitoa maelezo hayo wakati akijibu hoja za wabunge hususan wale wa kambi ya upinzani ambao tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti mwanzoni mwa mwezi uliopita, wamekuwa wakipinga malipo ya posho mbalimbali wanazolipwa watumishi wa umma.
“Serikali italitafakari kwa undani na kuangalia posho zipi hazina tija na zipi zina tija na manufaa ya kuongeza ufanisi ili ikiwezekana zihuishwe na kujumuishwa ndani ya mishahara au vinginevyo kama itakavyoonekana inafaa,” alisema Pinda.
Kauli ya Pinda aliyoitoa jana kuhusu posho, inatofautiana na ile aliyoitoa ndani ya Bunge wiki kadhaa zilizopita, wakati alipokuwa akijibu maswali ya wabunge kwenye kipindi maalum cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Katika kauli yake hiyo ya awali, Pinda alikaririwa akisema posho wanazolipwa watumishi wa umma wakiwamo wabunge zipo kisheria na hivyo taratibu zozote za kuziondoa zinapaswa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Mbali ya hilo, Pinda alitetea posho hizo akisema kwa kiwango kikubwa zilikuwa zikiwasaidia wabunge kuwakirimu wageni wanaowatembelea bungeni.
Katika hotuba yake ya jana, kabla ya kuhitimisha kwa kauli hiyo ya kutafakari na kuziangalia upya posho, Pinda alichambua aina mbalimbali ya posho wanazolipwa watumishi wa umma kisheria.
Akizungumzia kuhusu hoja ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye aliwashutumu viongozi kwa kushindwa kuchukua maamuzi magumu wakati akichangia mjadala wa hotuba yake, Pinda aliitetea serikali ya awamu ya nne akisema ndiyo iliyofanya mambo mengi kuliko zote zilizotangulia.
Akifafanua, Pinda alitoa mifano ya maamuzi magumu yaliyopata kuchukuliwa na serikali ya awamu ya nne kuwa ni kama yale ya ujenzi wa shule za kata na uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha Dodoma.
Mbali ya hayo Pinda alisema pia kwamba serikali katika kipindi hicho imejenga barabara nyingi, ikaanzisha mchakato wa Katiba mpya na akatoa mfano wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar kama moja ya maamuzi magumu yaliyopata kufanywa.
Hakuishia hapo, alikwenda mbele na kusema mfano mwingine wa maamuzi magumu ni ule wa kulivunja Baraza la Mawaziri ambao ulitokana na kujiuzulu kwa Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu.
Hata hivyo Pinda hakueleza lolote kuhusu mapendekezo ya Lowassa ya aina ya maamuzi magumu aliyokuwa akitaka serikali iyafanye kama yale ya kujenga upya na kupanua bandari za Mtwara, Tanga na Dar es Salaam.
Mbali ya hilo, Pinda hakueleza lolote kuhusu maoni mengine ya maamuzi magumu ya Lowassa ya kuitaka serikali ijenge upya Reli ya Kati na ile ya Tazara.
Hotuba hiyo ya majumuisho ya Pinda ilitanguliwa na nyingine iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Katika mchango wake wa hotuba ya Waziri Mkuu, Lukuvi alikiri kwamba karatasi za kujumlishia kura zilizotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, zilikuwa zinafutika kirahisi.
Lukuvi ambaye katika mchango wake huo alikuwa akijibu hoja za wabunge kuhusu hotuba hiyo hiyo Waziri Mkuu, alidai karatasi hizo zilikuwa na ubora wa hali ya juu ambao ulipaswa kuziwezesha kudumu kwa muda mrefu bila kufutika.
Alisema kwamba, kufutika kwa karatasi hizo kulitokana na waandishi kutogandamiza vizuri kalamu zao wakati wa kuandika idadi ya kura katika vituo vyao. Hata hivyo, hakusema kwanini, katika ubora huo aliosema, hali hiyo ya ‘kutogandamiza’ ilitokea nchi nzima.
Alikuwa akijibu hoja ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, aliyehoji ubora wa karatasi hizo, ambazo zilifutika mara tu baada ya kupiga kura, hivyo kufanya kazi ya kuhakiki idadi ya kura kuwa ngumu.
Hali hiyo ilimfanya Mbowe aitake serikali itangaze kuwa katika mazingira hayo, uchaguzi huo haukuwa huru na halali, kwani zoezi la kuhesabu lilikuwa na dosari ya msingi.
Akitetea kufutika kwa karatasi hizo, Lukuvi alisema, “fomu hizo zilitengenezwa kwa namna ambayo ukijaza fomu ya mwanzo (original) nakala sita zinajitengeneza zenyewe (self copying forms). Ili fomu hizo zitoe nakala zinazosomeka mjazaji anatakiwa akandamize kalamu ipasavyo.
“Kuna baadhi ya watendaji hawakukandamiza kalamu zao ipasavyo, na hivyo nakala zilizotengenezwa kutosomeka vizuri, ila original zilizotumika kujumlishia matokeo zilisomeka vizuri,” alisema Lukuvi.
Alisema kampuni iliyotumika kuchapisha karatasi na fomu za matokeo ni Kalamazoo Secure Solution ya Uingereza, na kwamba ilipatikana baada ya kushinda zabuni iliyotangazwa kwa kuzingatia sheria ya Ununuzi ya Umma ya mwaka 2004.
Alieleza kuwa kampuni hiyo ina uwezo mkubwa wa uzoefu wa miaka 100 kuchapisha nyaraka nyeti na ilichapisha karatasi hizo za kura katika nchi mbalimbali ikiwemo Nigeria, Kenya, Malawi, Uganda na Uingereza.
Pamoja na mambo mengine Lukuvi aliahidi kuwa serikali itato elimu ya kutosha kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015 ili wnaojaza fomu hizo wagandamize vizuri, wino usifutike.
Walioshindwa CCM wachelewesha matokeo
Akijibu hoja ya Mbowe kuhusu kuchelewa kutangaza matokeo katika maeneo mbalimbali nchini wakati wa uchaguzi wa mwaka 2010 hasa katika maeneo ambayo vyama vya upinzani, hususan CHADEMA, walikuwa wameshinda, Lukuvi alitoa mfano wa majimbo ya Nyamagana, Ilemela, Ubungo, Moshi Mjini, Kawe, Hai na Arusha Mjini.
Alisema hali hiyo ilitokana na ubishi wa wagombea walioshindwa au mawakala wao wakati wa kuhesabu kura, huku baadhi ya wagombea au mawakala wao wakitaka kura zihesabiwe upya, hata pale ilipokuwa dhahiri kwamba wameshindwa.
Muundo wa serikali
Kuhusu hoja ya Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa (CCM), aliyetaka serikali kuangalia upya muundo huo wa Ofisi ya Waziri Mkuu ili kupunguza urasimu na kupendekeza TAMISEMI kuwa Wizara inayojitegemea, Lukuvi alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 36 na 37, mamlaka ya kuunda wizara yamo mikononi mwa Rais.
Pamoja na Lowassa, wengine waliokuwa wametoa hoja hiyo ni Wabunge wa Viti Maalumu wa CHADEMA, Regia Mtema na Susan Lyimo, na Mbunge wa Mbulu Mustafa Akonaay (CHADEMA).
Ukubwa wa Baraza la Mawaziri
Hoja juu ya ukubwa wa Baraza la Mawaziri iliwasilishwa na Susan Lyimo aliyesema Baraza kubwa ni mzigo kwa taifa, kwani wajumbe 54 akiwemo Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Rais na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni wengi mno, wakati nchi zilizoendelea na zenye watu wengi zaidi kuliko Tanzania kama Marekani na Uingereza zina wizara zisizozidi 15.
Lukuvi aliendelea kusisitiza kuwa kwa mujibu wa Katiba ibara ya 36 na 37 mamlaka ya uteuzi wa viongozi wakuu, wakuu wa mikoa ni ya rais.
Alisema mamalaka hayo ynalenga kubadilisha vifungu vya katiba jambo ambalo linahitaji mchakato na kwa kuwa serikali inakusudia kufanya mabadiliko ya Katiba suala hilo litaangaliwa sanjari na maoni ya wadau wengine yatakayotolewa.
No comments:
Post a Comment