TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE
Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com
Thursday, June 23, 2011
Tucta wajiunga na upinzani
Msimamo wa Tucta umetolewa na Katibu Mkuu wake, Nicolaus Mgaya
.Wapinzani waitega serikali
.Wasubiri ufafanuzi, kutoa msimamo
Moto wa kupinga posho wanazolipwa wabunge za kuhudhuria vikao umeendelea kushika kasi na sasa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (Tucta) limeungana na kambi ya upinzani kuzipinga.
Msimamo wa Tucta umetolewa na Katibu Mkuu wake, Nicolaus Mgaya, ambaye ametaka kuondolewa kabisa kwa posho hizo na nyingine zinazolipwa kwa maofisa wa serikali kwa kuwa haziwanufaishi wananchi walio wengi.
Akizungumza na blog hii, Mgaya alisema kuwa hata kama suala hilo lipo kisheria, lakini sheria inaweza ikabadilishwa wakati wowote ili fedha hizo zikaelekezwa katika miradi ambayo itakuwa na manufaa kwa Watanzania wote badala ya sasa ambapo kundi dogo la watu wasiozidi asilimia mbili ya watanzania wote ndilo linalofaidika na posho hizo.
"Kwa mfano, katika bajeti ya safari hii, kiasi cha Sh. bilioni 987 zimetengwa kwa ajili ya kulipana posho na posho kama hizi mara nyingi wanalipwa maofisa wa ngazi za juu serikalini kuanzia ngazi ya ukurugenzi na kuendelea ikiwa ni pamoja na wabunge," alisema.
Alifafanua kuwa ikiwa posho hizo zitaondolewa na kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo kama vile afya, elimu, maji na kilimo, thamani ya fedha hizo itakuwa ni yenye tija kubwa zaidi kwa kuwa itawagusa wananchi wengi na hasa maskini.
Aidha, Mgaya aliitaka serikali kukifanyia kazi kilio cha Watanzania walio wengi cha kuhakikisha kuwa, posho hizo zinaondolewa kwa kuwa tayari hata baadhi ya mataifa wafadhili yameshaanza kuulizia juu ya suala hilo.
"Wiki hii (wiki iliyopita) tulikuwa na ugeni wa Rais Mstaafu wa Ujerumani, Profesa Horst Kohler, moja ya nchi ambazo hutupa misaada sisi watanzania na alihudhurua mdahalo mmoja uliofanyika hapa Dar es Salaam. Katika Mdahalo huo, naye aliligusia suala hili la posho kwa kuwa fedha za misaada wanazotupa zinatoka katika mifuko ya walipa kodi wao," alisema.
Alisema siyo vizuri kwa Wajerumani kama alivyosema rais wao mstaafu na wafadhili wengine wanaotoa fedha kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania wakasikia kwamba fedha wanazotoa kwa ajili ya maendeleo ya nchi zinaishia kwenye kulipana posho.
Mkazi wa Dar es Salaam, Juma Pembe, alipinga wabunge kulipwa posho hiyo akisema kuwa ni kazi kwa kuwa jukumu lao ni kutunga sheria.
Alihoji kama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anasema kiasi wanacholipwa wabunge ni kidogo, inakuwaje kwa watumishi wanaolipwa Sh. 135,000 kwa mwezi kuishi na kuzihudumia na familia zao.
Pembe alikosoa kauli ya Pinda kuwa fedha za wabunge zinaishia kwa wapiga kura na kuhoji ni wapiga kura wangapi wanawagawia fedha hizo.
UPINZANI WASUBIRI KESHO
Katika hatua nyingine, Kambi ya Upinzani Bungeni, imesema itaeleza hatua za ziada itakayochukua iwapo wakati wa kuhitimisha mjadala wa bajeti kesho, serikali haitatoa ufafanuzi bungeni jinsi itakavyofanya mabadiliko katika mfumo wa posho katika utumishi wa umma.
Kambi hiyo pia imeelezea ilivyokerwa na kauli iliyotolewa na Pinda ya kuhalalisha posho kwa wabunge kwamba zinahitajika kwa ajili ya kuwapa watu wanaowaomba fedha nje ya ukumbi wa Bunge.
Imesema kauli hiyo inahamasisha siasa za fadhila.
Ilalamikia kauli ya Pinda kuwa wabunge wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanamezea mate posho hizo kuwa inalenga katika kujaribu kuonyesha kwa umma kwamba hoja ya kutaka mabadiliko katika mfumo wa posho ni ya wabunge wachache.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma,Katibu wa Wabunge wa Upinzani, John Mnyika, alimtaka Pinda kufuta kauli zake hizo,
"Na iwapo Bunge halitatoa ufafanuzi ikiwemo hatua mahususi kuelezwa bungeni kuhusu serikali itakavyoweza kufanya mabadiliko katika mfumo wa posho katika utumishi wa umma wakati wa kuhitimisha mjadala wa bajeti, tutakaa kama Kamati ya wabunge wa chama kwa mujibu wa kanuni za Kudumu za Bunge kifungu namna 109 na 110 kama sehemu ya kuweka msimamo wa pamoja kuhusu bajeti na kueleza hatua za ziada ambazo tutachukua kuhusu posho hizo (Sitting allowance) na ubadhirifu mwingine,” alisema Mnyika.
Akizungumza hoja ya kutaka posho zifutwe, Mnyika alisema kuwa hoja hiyo imeainishwa katika ilani yao ya uchaguzi ya Agosti mwaka jana kifungu namba 5.5., kipengele cha tano kimeelezea jinsi CCM inavyotenga kiwango kikubwa kwa ajili ya posho.
Alisema ilani hiyo imefafanua lengo la kupunguza posho hizo kwa zaidi ya asilimia 80 zikiendana na ongezeko la mishahara kwa watumishi wa umma kuendana na ujuzi, nafasi na wajibu.
Aliongeza kusema kuwa suala hilo limezungumzwa katika vikao vya chama hicho na kuainishwa katika bajeti mbadala ya upinzani iliyosomwa na Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe.
Mnyika alisema posho hiyo haitajwi katika katiba ya nchi wala sheria yoyote na kwamba posho hiyo imetolewa kwa mujibu wa kifungu namna 10 (d), nne ambacho kinampa ridhaa Rais kutoa poshi zingine kwa Wabunge.
Alisema mamlaka hiyo ndiyo iliyofanya kutolewe waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi Ofisi ya Rais wa Oktoba 25, mwaka jana wenye kumbukumbu CAB 111/338/01/83.
Alimtaka Rais Jakaya Kikwete kufuta posho hizo haraka badala ya kusubiri mabadiliko ya kisheria na kikatiba kama Pinda alivyoeleza bungeni.
PINDA AKOSOLEWA
Katika hatua nyingine, Chadema kimesema Pinda sio mtoto wa mkulima kwa kuwa ameonyesha mfano mbaya kwa Watanzania kutokana na kutetea posho za vikao anazolipwa Mbunge pamoja na watumishi wengine wa serikali.
Kimesema awali kiliamini kuwa Pinjda ni mtoto wa mkulima, lakini kutokana na kauli aliyoitoa bungeni wiki iliyopita, ameonyesha kuwa anakumbatia matajiri na kujali maslahi ya watu wachache.
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chadema, Erasto Tumbo, aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa kauli ya Pinda imeonyesha dharau kubwa Watanzania zaidi ya milioni 40.
Kutokana na kuali hiyo, Chadema kimemtaka Pinda kutafuta jina lingine la kujiita badala ya mtoto wa mkulima.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment